Mkurugenzi Mtendaji,Amana Bank Dk Muhsin Masoud katika picha ya pamoja wakionesha mikata baada ya kusaini na Dk. Diana B. Putman, Naibu Mkurugenzi wa USAID katika Idara ya Afrika.
Dar es Salaam: Oktoba 7, 2019, Serikali ya Marekani, kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), imesaini mkataba wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 10 na Amana Bank. Lengo la DCA ni kuimarisha uwezo wa benki katika kutoa fedha kwa shughuli zinazohusiana na kilimo na biashara ndogondogo na za kati na kwa biashara zinazomilikiwa na wanawake na vijana nchini Tanzania.
Wakati wa hafla hii, Dk. Diana B. Putman, Naibu Mkurugenzi wa USAID katika Idara ya Afrika alisema, “Mkataba huu umekusudia kuimarisha uwezo wa Benki ya Amana kutoa fedha kwa Kilimo biashara nchini Tanzania. Hivyo, tunatarajia utachangia katika ukuaji endelevu wa biashara zinazohusiana na kilimo.”
Mbali na kufadhili upatikanaji wa mikopo, mkataba huu umeongeza upatikanaji kwa wateja na mikoa ya Tanzania, ikiwemo Zanzibar. Wakati USAID inashirikiana na benki za Kiislamu katika maeneo mengine duniani, mkataba na Amana Bank ni wa kwanza kwa Benki ya Kiislamu Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Dk Muhsin Masoud, Mkurugenzi Mtendaji, Amana Bank alisema, “Mara nyingi mtaji hutajwa kama sababu kuu inayorudisha nyuma ukuaji wa biashara katika sekta ya kilimo hasa katika biashara ambazo zinazomilikiwa na wanawake na vijana katika nchi nyingi zinazoendelea. Vizuizi vikuu ni pamoja na ukosefu wa umiliki wa dhamana, kwani kwa sehemu kubwa mila na desturi hazijazingatia haki ya mwanamke katika kumiliki mali, vilevile kukosekana kwa historia ya ukopaji na marejesho. Hivyo basi makubaliano haya, yataenda kusaidia kupunguza changamoto hizi”
Serikali ya Marekani na Amana Bank kwa jumla tunaunga mkono maendeleo ya biashara na mchango wa sekta binafsi katika kuchangia maendeleo ya Tanzania na uwezo wa kufikia hadhi ya kujitegemea.